10 Novemba 2025 - 17:11
Ayatullah A‘rafi: Hatua Zote Kuhusu Wahamiaji Zinapaswa Kuchukuliwa kwa Mtazamo wa Maadili na Uislamu

Ayatollah A'rafi aliashiria juu ya umuhimu wa uongozi maalumu katika masuala ya wahamiaji, akitaja mji wa Qom kuwa ni eneo lenye umuhimu mkubwa linalohitaji mpango thabiti wa kiutamaduni, usimamizi wa karibu, na juhudi za kudumisha utambulisho wa kidini na kijamii wa wahamiaji.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (a.s) — ABNA, Ayatullah Alireza A‘rafi, Mkurugenzi Mkuu wa Vyuo vya Dini (Hawza) nchini Iran, amesema kuwa masuala ya uhamiaji na wahamiaji wasio Wairani yanahitaji hekima ya pamoja, mtazamo wa kiuhuru wa Kiislamu na kimaadili, pamoja na mpango wa kitaifa unaolinda umoja wa Kiislamu.

Kauli hiyo aliitoa katika kikao chake na Nader Yar-Ahmadi, Mkuu wa Kituo cha Masuala ya Raia wa Kigeni na Wahamiaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kilichofanyika siku ya Jumapili (09 Novemba ) katika ofisi ya uongozi wa vyuo vya dini.

Ayatullah A‘rafi alieleza kuwa suala la uhamiaji lina vipengele vya kimaadili, kibinadamu, kitaifa, kisiasa, kiutamaduni na kijamii, hivyo serikali na bunge vinapaswa kulizingatia kwa mtazamo mpana na wa kina.

Amesema: “Katika masuala haya nyeti, ni lazima sura ya Iran na Mapinduzi ya Kiislamu ilindwe katika uwanja wa kimataifa, na kila hatua ichukuliwe kwa hekima ya pamoja, dhamira ya kitaifa na maono ya kimaadili.”

Akinukuu matukio ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongezeka kwa nafasi ya fikra na kiroho ya Iran baada ya vita vya siku 12 dhidi ya utawala wa Kizayuni, Ayatullah A‘rafi alisisitiza haja ya maamuzi yanayoendana na nafasi ya kiutamaduni, kiuchumi na kimapinduzi ya Iran kuhusu masuala ya wahamiaji.

Aidha, alihimiza umuhimu wa:

  • Kuwaunganisha wahamiaji halali na jamii,
  • Kuzuia migongano ya kitamaduni na kijamii,
  • Kuweka mipango sahihi ya taasisi za kidini na kiutamaduni,
  • Kutambua na kusaidia vipaji na wahamiaji wenye elimu na nafasi ya kipekee,
  • Kulinda utambulisho wa kidini na kimaadili wa vizazi vipya vya wahamiaji, na
  • Kuwajengea nafasi ya kushiriki ipasavyo katika jamii ya Kiislamu.

Ayatullah A‘rafi alibainisha kwamba vyuo vya dini vinapaswa kuwa kiini cha ushirikiano wa fikra na utamaduni, ili kutumia ipasavyo uwezo wa taasisi mbalimbali katika kulijenga taifa.

Aliongeza: “Kila uamuzi na hatua kuhusu wahamiaji lazima iwe na mtazamo wa kuimarisha umoja wa kijamii na wa kitaifa, ili uhamiaji uwe fursa ya maendeleo, mshikamano na kuinua maadili ya kiutamaduni na kimaadili.”

Mwisho, alisisitiza umuhimu wa uongozi maalumu katika masuala ya wahamiaji, akitaja mji wa Qom kuwa ni eneo lenye umuhimu mkubwa linalohitaji mpango thabiti wa kiutamaduni, usimamizi wa karibu, na juhudi za kudumisha utambulisho wa kidini na kijamii wa wahamiaji.

Kwa upande wake, Nader Yar-Ahmadi alieleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuratibu na kurudisha wahamiaji wasio halali kwa njia salama, kwa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na uhamiaji, sambamba na kutambua wahamiaji wanaostahili kurejeshwa na kupunguza athari za kijamii na kiuchumi za uwepo wao usio halali nchini.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha